Thursday, May 26, 2016

TAMASHA LA NYAMA CHOMA LAJA!

 Mkuu wa Kitengo cha Burudani na Digitali wa Tigo, Paulina Shao (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuhusu tamasha la nyama choma litakalofanyika  Viwanja vya Leaders kesho kutwa Jumamosi Mei 28, 2016 jijini Dar es Salaam, ambapo mwanamuziki Ben Pol atatoa burudani kwa udhamini wa kampuni ya Tigo. Kulia ni Mratibu Mkuu wa Tamasha hilo, Carol Ndosi na katikati ni mwanamuziki Ben Pol.
 Mratibu Mkuu wa Tamasha hilo, Carol Ndosi (kulia), akizungumza katika mkutano huo.
 Mwanamuziki, Ben Pol (katikati), akizungumza katika mkutano huo.
 Mtaalamu wa Kidigitali, Samira Baamar (kushoto), akichangia jambo kwenye mkutano huo.
Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.


Na Dotto Mwaibale

Kampuni inayooongoza kwa maisha ya kidijitali Tigo Tanzania leo imekubali kumdhamini mwanamuziki nguli na mtunzi wa nyimbo za muziki, Bernard Michael Paul Mnyang'anga, maarufu kama ‘Ben Pol’ kuburudisha katika tamasha la mwaka huu la Nyama Choma.

 Tamasha hilo ambalo linafanyika kwa mwaka wa tano sasa ni moja ya tamasha maarufu linalovutia watu wengi kutoka maeneo yote ya Dar es Salaam litafanyika kwenye viwanja vya Leaders Jumamosi Mei 28, 2016. 
 Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Mkuu wa Tigo wa masuala ya Dijitali Paulina Shao  alisema kuwa  kumuunga mkono Ben Pol kunaonesha  kuendelea kujikita kwa Tigo katika  kuwekeza katika kusaidia  sekta ya muziki ya ndani kwa kuhakikisha  wasanii  wanawezeshwa  kufikia viwango vya juu katika kazi zao.

“Kama kampuni ya maisha ya kidijitali, Tigo inatambua  mchango muhimu wa wasanii wa Tanzania  wanaoutoa katika sekta ya burudani. 

Hii ndio maana  tumewekeza kwa kiwango kikubwa  kuwasaidia wasanii  hususani wanamuziki  wa ndani katika kuhakikisha wanafahamika katika masoko ndani ya nchi, kikanda na kimataifa kwa kutumia majukwaa ya kidijitali yanayokuwepo na kushiriki  matukio mbalimbali  na hivyo kuongeza  mauzo ya  muziki wao  pamoja na nembo zao,” alisema Shao.

Aidha akiishukuru Tigo kwa uungwaji mkono huo, Ben Pol  aliisifu Tigo kwa juhudi  inazofanya bila kuchoka  katika kukuza  ukuaji wa  sekta ya muziki wa ndani  kupitia Jukwaa la Muziki  la Tigo.

“Ninaishukuru sana Tigo  kwa uungwaji mkono ambao ni muendelezo wa mtiririko wa  programu ambazo imezianzisha  ili kuinua maisha ya wasanii wachanga wa Tanzania,” alisema Ben Pol na kutoa changamoto kwa wasanii wanaoibukia kuwa wasione aibu  kuomba msaada  kutoka kwa mashirika kama Tigo.

Nguli huyo wa muziki wa Bongo Flava  kwa hivi sasa anatamba na  kibao ‘MoyoMashine’ ambayo aliitoka hivi karibuni.

Ben Pol ni miongoni mwa wasanii  wanaonufaika na jukwaa la Muziki la Tigo  ambalo lilianzishwa mwaka 2015 likiwa na lengo la  kuiunga mkono sekta ya muziki Tanzania  kwa kuwasaidia wasanii wa ndani  kupata kipato zaidi kutokana na mauzo ya  kazi zao  na kuwawezesha kufahamika katika masoko ya kimataifa  kupitia majukwaa hayo ya kidijitali  kama vile Music portal na Deezer, ambayo ni majukwaa ya kimataifa yaliyo kwenye mtandao yakiwa na  nyimbo kutoka sehemu mbalimbali  duniani  zaidi ya  milioni 36.MWANAHABARI MAKONGORO AAGWA!

 Picha ya Mwanahabari Makongoro Oging' enzi za uhai wake.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers alikokuwa akifanyia kazi Makongoro Oging', Eric Shigongo akitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza lenye lenye mwili wa marehemu Oging' wakati wa kuagwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ilala ya Amana Dar es Salaam mchana wa leo.
 Mmiliki wa Blog ya Michuzi, Issa Michuzi akitoa heshima za kwa mwili wa marehemu.
 Mhariri wa Habari wa Gazeti la Champion, Salehe Ali akitoa heshima za mwisho kwa marehemu.
 Waombolezaji wakiwa na huzuni wakati wa kuaga mwili wa mpendwa wao Makongoro.
 Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha ITV. Samu Mahela akitoa heshima za mwisho.
 Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri wa Habari Tanzania (TEF), Absalom Kibanda akiwa kwenye shughuli hiyo ya kumuaga Makongoro Oging'
 Ndugu yake na Makongoro Oging' akilia wakati wa kumuaga mpendwa wake Makongoro.
 Ndugu jamaa na marafiki wakiwa kwenye uagaji wa mpendwa wao.
 Uagaji ukiendelea.
 Mtoto wa marehemu akimuaga baba yake 'hakika ni huzuni kubwa'
 Majane wa marehemu akiwa hajiwezi baada ya kumuaga mume wake.
 Mhariri wa habari wa gazeti la jambo leo alilokuwa akiandia marehemu Oging' Elvan Stambuli akilia kwa uchungu wakati wa kumuaga Makongoro.
 Baba mlezi wa Makongoro Oging ambaye alimsomesha, akizungumza na wanahabari.
Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Makongoro kulipeleka kwenye gari kabla ya kuanza kwa safari ya kwenda mkoani Mara.
Jeneza likiingizwa kwenye gari tayari kwa safari.


Sunday, May 8, 2016

WAZANZIBAR WEKEZENI NYUMBANI!

Nembo ya ZADIA
Na Mwandishi wetu Washington 
Wazanzibari waishio nchi za nje wametakiwa kuwekeza nyumbani kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya taifa.
Wito huo ulitolewa jana na maofisa kutoka Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zaznzibar (ZSSF) wakati wakizungumza na Wazanzibari waishio nchini Marekani.
Akizungumza kwenye mkutano huo uliondaliwa na Jumuiya ya Wazanzibari waishio nchini Marekani (ZADIA), Meneja wa Mipango na Uwekezaji kutoka ZSSF Bwana Khalifa Muumin Hilal alisema kuwa Taasisi yake ina miradi kadhaa ya uwekezaji inayoendeshwa kwa ushirikiano na Benki ya Watu wa Zanzibar, na kwamba inawahamasisha Wazanzibari waishio Ughaibuni kuwekeza katika miradi hiyo.
Miongoni mwa miradi hiyo ni mradi wa nyumba za kisasa katika eneo la Mbweni, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar ambao ujenzi wake tayari umeanza na unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miaka mitatu.
Bwana Hilal alifafanua kuwa eneo hilo litakuwa na majengo ya nyumba za kuishi yenye urefu wa ghorofa saba, ambapo kila ghorofa itakuwa na nyumba mbili.
"Kutakuwa na nyumba za vyumba viwili, vitatu na vinne" alifafanua Meneja Hilal, na kuongeza kuwa nyumba hizo zitapatikana kwa bei nafuu.

Sunday, March 13, 2016

MWANZA WAMLILIA DIAMOND!

Staa Diamond Platnumz
Na:George Binagi-GB Pazzo @BMG.
Staa wa muziki nchini Naseeb Abdul Juma a.k.a Diamond Platnumz ametakiwa kutoka Jijini Dar es salaam na kurejea Mkoani Kigoma alikozaliwa, ili kuwasaidia Wasanii chipukizi katika Mkoa huo.

Mbali na Diamond, Staa mwingine alietajwa ili atoke Jijini Dar es salaam na Kurejea Mkoani kwake ni Farid Kubanda a.k.a Fid Q, ambae ametakiwa kurejea Jijini Mwanza ili kusaidia kuukuza muziki wa Mwanza.

Mbali hao mastaa hao ambao wametajwa live majina yao, pia mastaa wote waliohamishia shughuli zao za sanaa Jijini Dar es salaam wametakiwa kurejea katika Mikoa yao ili kuondoa mrundikano wa wasanii katika Jiji hilo.

Hayo yalisemwa juzi ijumaa Jijini Mwanza na Msanii Chipukizi Joseph Stanford a.k.a Rich4D, katika hafla ya kumpongeza kwa ushujaa wake wa kutembea kwa miguu kutoka Jijini Mwanza hadi Jijini Dar es salaam, kwa ajili ya Kumpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kutambua mchango wa wasanii nchini na kuwajumuisha katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

"Wasanii wakubwa watoke Jijini Dar na warudi Mikoani kwao ili wawasaidie wasanii chipukizi wa Mikoani. Diamond arudi Kigoma. Fid Q arudi Mwanza. Hii itaondoa mrundikano wa wasanii wakubwa Dar na hivyo kupeleka fursa za sanaa mikoani". Alisema Rich4D.

Matembezi ya Miguu ya Msanii Rich4D yalianza Januari 16,2016 yakihusisha mikoa minane sawa na Kilomita 1,200 na yalifikia tamati Februari 10,2016, lakini adhma yake ya kuonana na rais haikuweza kutimia baada ya rais kuwa katika majukumu mengine ya kitaifa ambapo aliekuwa Katibu Mkuu Ombeni Sefue aliahidi msanii huyo kuonana na rais.

Wadau mbalimbali waliosaidia kufanikisha matembezi hayo akiwemo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana Raphael Shilatu pamoja na Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Stanslaus Mabula, wameyapongeza matembezi hayo na kusema kuwa ni ya kizalendo ambapo wamemuomba Katibu Mkuu Mpya, Mhandisi John Kijazi kuhakikisha ahadi aliyoiacha Sefue inatimia ili msanii Rich4D afanikiwe kuonana na rais magufuli.
Staa Fid Q
Msanii Rich4D anaechipukia kwa kasi Jijini Mwanza ambapo tayari anatamba na ngoma mbili ambazo ni "Tawile" na "Huniwezi".
                    

Wednesday, February 24, 2016

NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI, KATIBU MKUU WALA VIAPO KUIONGOZA TUME YA UTUMISHI YA JESHI LA POLISI NA MAGEREZA.


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Injinia Hamad Masauni akila kiapo cha kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi ya Jeshi la Polisi na Magereza mbele ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu, Shabani Lila (kushoto) jijini Dar es Salaam leo. Tume hiyo inashughulikia masuala ya kiutumishi kwa askari Polisi na Magereza. Katikati ni Msajili wa Mahakama Kuu, Ilvin Mugeta. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira akila kiapo cha kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi ya Jeshi la Polisi na Magereza mbele ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu, Shabani Lila (kushoto) jijini Dar es Salaam leo. Tume hiyo inashughulikia masuala ya kiutumishi kwa askari Polisi na Magereza. Katikati ni Msajili wa Mahakama Kuu, Ilvin Mugeta. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Injinia Hamad Masauni (kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu, mara baada ya Jaji huyo kuwaapisha kuwa viongozi wa Tume ya Utumishi ya Jeshi la Polisi na Magereza katika tukio lililofanyika Mahakamani hapo, jijini Dar es Salaam leo. Injinia Masauni katika Tume hiyo amekuwa Makamu Mwenyekiti, na Meja Jenerali Rwegasira amekuwa Katibu. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

KABLA HAUJAFANYA MAGENDO JULIZE MASWALI HAYA!

Afisa Mdhamini wa ZSTC Pemba Abdulla Ali Ussi akitoa maelezo baada ya Magunia ya Karafuu Kavu kukamatwa na Kikosi cha KMKM katika Ufukwe wa Bahari ya Chanjaani Mtambwe ambazo zilikuwa katika harakati za kutaka kusafirishwa kwa njia ya Magendo. Anaemsikiliza ni Kamanda wa KMKM zone ya Pemba, Silima Hija Hija.
NA ALI MOHAMED ZANZIBAR

Magendo ni vitendo viovu vinavyohusisha uingizaji au usafirishaji wa bidhaa au mazao kwa njia zisizo halali/kisheria kwa lengo la kukwepa kodi na kukiuka sheria ambapo ni njia haramu ya kufanya biashara. Sababu kuu za magendo ni tamaa ya utajiri, ujinga na kukosa uzalendo.

Ni dhahiri kuwa magendo yana athari kubwa kwa maendeleo ya nchi na Wananchi wake, huikosesha serikali mapato ambayo ndio yanayohitajika katika kuimarisha huduma za jamii kama vile utoaji wa elimu, afya, maji safi na salama, ujenzi wa miundombinu ya barabara na huduma nyengine muhimu.

Karafuu ni zao kuu la uchumi wa Zanzibar linalosaidia upatikanaji wa fedha za kigeni na kuiwezesha Serikali kuimarisha huduma za jamii. Katika kipindi cha miaka ya 1980 na 2010 zao hili lilikuwa katika changamoto kubwa ya kusafirishwa kwa magendo. Baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu walikuwa wakisafirisha zao hili kwa magendo kwenda katika nchi za jirani.

Katika wakati huo usafirishaji magendo wa zao la karafuu ulikuwa mkubwa kiasi cha kuzifanya nchi hizo za jirani kuwa wauzaji wakubwa wa zao la karafuu kwa zaidi ya tani 2,000 katika soko la dunia huku ikizingatiwa kuwa katika nchi hizo hakuna mikarafuu inayolimwa.

Wakati nchi hizo zikionekana kuuza karafuu kwa kiwango hicho, uzalishaji wa zao hilo kwa Zanzibar ulishuka kutoka tani 9,952 hadi tani 2673 katika kipindi cha miaka kumi, sababu moja ikiwa ni karafuu za Zanzibar kusafirishwa kwa magendo kwenda katika nchi hizo za jirani.
Katika kipindi hicho cha mwaka 2000 hadi 2010, Zanzibar ilipoteza kiasi cha dola za kimarekani milioni 16, sawa na TZS bilioni 34.7 kutokana na usafirishaji karafuu kwa magendo.
Kwa mujibu wa sheria ya ZSTC ya mwaka 2011 kifungu cha 9 (a) Wakulima na Wafanyabiashara wa zao hilo la karafuu wanatakiwa kuuza karafuu zao Serikalini tu kupitia Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) ambayo ni taasisi pekee iliyopewa mamlaka ya kununua na kuuza karafuu, hivyo kufanya magendo ya karafuu ni makosa.
Kulikuwa na sababu nyingi zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya watu ikiwemo suala la bei ya karafuu kuwa ndogo na kusababisha watu kuamua kuziuza karafuu zao kimagendo nje ya nchi kwa lengo la kutafuta bei nzuri.
Kwa lengo la kuimarisha, kulinda ubora na kuwahamasisha Wakulima kuuza karafuu zao Serikalini kupitia vituo vya ununuzi vya ZSTC badala ya kusafirisha kwa magendo, mikakati mbali mbali ilipangwa na kutekelezwa na Serikali.

Mwaka 2011 Serikali ilitoa ahadi na kuitekeleza ahadi hiyo ya kuwalipa Wakulima wa zao la karafuu asilimia 80 (80%) ya bei ya karafuu ya soko la dunia. Karafuu za daraja la kwanza zinanunuliwa kwa bei ya TZS 14,000 kwa kilo badala ya TZS 5,000 kwa kilo, bei iliyokuwepo mwaka 2010.  Ongezeko hili ni sawa na asilimia 180.

Kadhalika, vituo vipya vya ununuzi na uuzaji wa karafuu vimejengwa, vituo vya zamani vimekarabatiwa ambapo idadi kamili ya vituo vyote ni 35 Unguja 3 na Pemba 32, huduma zote muhimu zimeimarishwa kwenye vituo hivyo na ulinzi pia umeimarishwa zaidi katika kudhibiti magendo.

Mkakati mwengnie uliochukuliwa ni kwa Shirika la ZSTC kujipanga vyema katika suala la upatikanaji wa kifedha kwa wakati na kulipa fedha taslim kwa Wakulima wa zao la karafuu na kuhakikisha hakuna Mkulima anaekopwa karafuu zake anapokwendwa kuuza.

Utekelezaji wa mikakati hiyo imesaidia sana kufanikiwa kudhibiti magendo ya karafuu, hivi sasa Wananchi wanauza karafuu zao katika vituo vya ununuzi vya ZSTC. Ni jambo la kuwashukuru na kuwapongeza Wakulima, Wananchi na Vikosi vya Ulinzi na Usalama kwa kazi nzuri walioifanya ya kushirikiana na Serikali katika kupambana na magendo ya karafuu.

Pamoja na mikakati na jitihada hizo zilizochukuliwa na Serikali kudhibiti magendo ya  karafuu kufanikiwa kwa kiwango kikubwa lakini inaonekana kuwa bado wapo watu wachache wanaendeleza biashara hiyo haramu. Katika msimu wa mavuno mwaka 2015/2016 gunia 33 za karafuu kavu na gunia 31 za makonyo zimekamatwa ambazo zilikuwa zinasafirishwa nje.

Lakini kabla Mkulima hajafikiria suala la kuuza karafuu zake kwa njia ya magendo, anapaswa kwanza ajiuulize masuali yafuatayo;-
Ni nini anachotaka zaidi ilhali karafuu zimeongezwa bei na bei hiyo ni kubwa zaidi ya huko anakokwenda kuuza kwa magendo?
Pia kwa nini anafanya magendo llhali pamoja na bei nzuri lakini pia faida ya karafuu ikirudishwa ndani ya nchi ndio hupatikana elimu bora kwa mwanawe, afya bora kwake, barabara nzuri kwa wote, maji safi kwa kila mtu na maendeleo kadhaa wa kadhaa?
Inakuwaje mtu anajitia katika magendo ya karafuu ilhali uwezekano wa kupoteza maisha yake ni mkubwa au uwezekano wa kukamatwa na kufungwa na kupoteza utumishi wake kwa familia yake na kuitia katika mateso, kwa nini anafanya hivyo?
Ni kwa sababu gani za msingi watu ambao wanauwezo wa kupata kiasi kikubwa cha fedha kwa kuuza karafuu zao serikalini waingie katika tombola ya kukosa kabisa kwa kujaribu kuingia kwenye magendo na kuhatarisha mali zao kwa kuzama baharini au kufilisiwa na kubaki katika umaskini kwa kukosa fedha za Serikali na zile ambazo walizitarajia kuzipata kwa kuuza magendo huko nchi za jirani?
Ni wazi kuwa anachokosa mtu huyo ni uzalendo na uwezo mzuri wa kufikiri.​

WAZIRI KITWANGA, MASAUNI NA WATENDAJI WAKUU JESHI LA MAGEREZA WAPANGA MIKAKATI KULIBORESHA JESHI HILO.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto) akizungumza na Watendaji Wakuu wa Jeshi la Magereza nchini pamoja na Wakuu wa Idara wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuhusu masuala mbalimbali ya utendaji wa kazi ndani ya Jeshi hilo na Wizara kiujumla. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Wakwanza upande wa kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira akifuatiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Simba Yahya. Kulia ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP), John Minja. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto meza kuu) akizungumza na Watendaji Wakuu wa Jeshi la Magereza nchini pamoja na Wakuu wa Idara wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuhusu masuala mbalimbali ya utendaji wa kazi ndani ya Jeshi hilo na Wizara kiujumla. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Kulia meza kuu ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Injinia Hamad Masauni. Wapili upande wa kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira akifuatiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Simba Yahya. Wapili kushoto ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini (CGP), John Minja akifuatiwa na Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Jeshi hilo, Dk. Juma Malewa. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.


Sunday, February 21, 2016

WAZIRI MKUU WA SOMALIA AZUIWA AIRPORT.

Taarifa kutoka vyombo vya habari vya somalia zinasema kuwa Waziri mkuu wa nchi hiyo,Abdirashid Sharmarke, alishikiliwa kwa muda juzi katika kiwanja cha ndege wa Jomo Kenyatta , Nairobi nchini kenya wakati akiwa anafanyiwa ukaguzi wa usalama.
Taarifa hizo zinasema kuwa afisa usalama kufanya ukaguzi kwa sababu ndege aliyokuja nayo ya kukodi ya Somalia ilikuwa haijafanyiwa ukaguzi wa lazima katika uwanja wa ndege wa Wajir nchini Kenya.
Hata hivyo ripoti hiyo inasema ndege iliamua kuondoka na kuwaacha maafisa hao wakiwa wameshikiliwa kwa saa kadhaa.
Kenya imekuwa ikiisalidia somalia kupambana na kundi la kigaidi la la al-shabab lakini katika nchi zote mbili kumekuwa na mvutano baina ya serikali mbili juu ya kundi hilo al shabab na kusababisha mauaji ya baadhi ya askari wa kenya kuuawawa Somalia mwezi uliopita.

140 wameuawa kwa milipuko ya mabomu katika miji ya Homs na Damascus nchini Syria.

Takriban watu 140 wameuawa kwa milipuko ya mabomu katika miji ya Homs na Damascus nchini Syria, waangalizi na vyombo vya habari vya serikali vimeeleza.
Takriban milipuko minne ilitokea katika eneo la Sayyida Zeinab mjini Damascus na kuua takriban watu 83. Awali mjini Homs Watu 57 wengi wao raia waliuawa kwa mashambulizi ya mabomu yaliyokuwa yametegwa kwenye magari mawili.
Wanamgambo wa Islamic State wamekiri kutekeleza mashambulizi hayo katika miji hiyo miwili.
Wakati huo huo, Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, John Kerry amesema makubaliano ya muda yamefikiwa kati Marekani na Urusi kuhusu suluhu ya mgogoro wa Syria.

MWANZA YACHANUA MBAWA KWA USHONAJI NGUO.

 Mkurugenzi wa Mikalea Professional Tailors, Idda Adam, ambao ni washonaji wa Mavazi ya aina mbalimbali Jijini Mwanza, akionyesha mavazi mbalimbali yanayopatikana ofisini kwake, Mtaa wa Ghana GreenView, Nyamanoro Jijini Mwanza.


"Sisi tunahusika na suala la urembo pamoja na ushonaji wa mavazi ya kila aina ikiwemo mavazi ya Kitchen Party pamoja na Harusi (Wanaume na Wanawake). Tumelenga kukata kiu ya ushonaji wa mavazi kwa wakazi wa Jiji la Mwanza ambao awali walikuwa wakishona nguo zao nje ya Mwanza;

Pia tunawatumia wabunifu wa mavazi kutoka Jijini Mwanza na kutumia ujuzi wetu wa ushonaji na hivyo kuzalisha mavazi ambayo wateja wetu wamekuwa wakiyafurahia". 
Idda Adam anasema Mikalea Professional Tailors wabunifu na washonaji wa mavazi ya kila aina.
Mavazi mbalimbali kutoka Mikalea Professional Tailors ambao ni Mabingwa wa Ushonaji wa Mavazi ya aina mbalimbali Jijini Mwanza
Mavazi mbalimbali kutoka Mikalea Professional Tailors ambao ni Mabingwa wa Ushonaji wa Mavazi ya aina mbalimbali Jijini Mwanza.
Mkurugenzi akiteta jambo na fundi wake 
Mafunzi Ushonaji wa Mikalea Professional Tailors ambao ni Mabingwa wa Ushonaji wa Mavazi ya aina mbalimbali Jijini Mwanza wakiendelea na shughuli za ushonaji.
George Binagi-Binagi Pazzo (Kushoto) akizungumza na Idda Adam (Kulia) ambae ni Mkurugenzi wa Mikalea Professional Tailors ambao ni Mabingwa wa Ushonaji wa Mavazi ya aina mbalimbali Jijini Mwanza.

POLISI WAFUNGA KIKAO KAZI CHAO, Tayari kwa kulinda Raia.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, akizungumza wakati wa kufunga kikao  kazi cha Maafisa Maandamizi wa Jeshi la Polisi katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Wapili kulia meza kuu ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira (kulia), akipokelewa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Ilala, SACP Lucas Mkondya, alipofika kufunga kikao  kazi cha Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu (kulia), akimpongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, mara baada ya Katibu Mkuu huyo kumaliza kutoa hotuba ya kufunga Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi hilo uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

MBUNGE VITI MAALUM CHADEMA AZINDUA BONGE LA OFISI.

Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake Chadema Taifa BAWACHA na Mbunge Viti Maalumu Taifa Grace Tendega (katikati), akizindua ofisi Mpya ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza Chadema, Susan Masele (Kulia). Kushoto ni Paschazia Renatus ambae ni Katibu wa Bawacha Mkoa wa Mwanza.


Akizungumza katika Uzinduzi huo, Tendega alipongeza uwepo wa ofisi hiyo ambayo itakuwa ikisikiliza kero za wananchi bila kujalisha itikadi zao za kisiasa kwa ajili ya kupokea hoja za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi ikiwemo kuzisemea bungeni.

"...Kazi ya Mbunge siyo kugawa hela. Kazi ya Mbunge ni kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua. Na mimi niseme nitakuwa mwakilishi bora na hapa tumeanza tu ambapo katika ofisi hii nitakuwa napokea na kusikiliza kero za wananchi na kwenda kuzisemea bungeni... Alisema Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza Chadema, Susan Masele.

Ofisi hiyo inapatikana Mtaa wa Ghana Green View, Kata ya Nyamanoro, Jimbo la Ilemela Mkoani Mwanza. Ndani yake pia kuna Ofisi ya BAWACHA Mkoa wa Mwanza.
Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake Chadema Taifa BAWACHA na Mbunge Viti Maalumu Taifa Grace Tendega (katikati) jana February 20,2016 akizindua ofisi Mpya ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza Chadema, Susan Masele. Kushoto ni Paschazia Renatus ambae ni Katibu wa Bawacha Mkoa wa Mwanza.
Kulia ni Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake Chadema Taifa BAWACHA na Mbunge Viti Maalumu Taifa Grace Tendega akiwa pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza Chadema, Susan Masele.
Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake Chadema Taifa BAWACHA na Mbunge Viti Maalumu Taifa Grace Tendega akizungumza katika uzinduzi wa ofisi ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza (Chadema).
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza Chadema, Susan Masele akizungumza katika uzinduzi wa ofisi ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza (Chadema).
Mwenye Kinasa sauti ni Damas Kimenyi ambae ni Katibu wa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza (Chadema), akizungumza katika uzinduzi wa ofisi ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza (Chadema).
Madiwani wa Chadema Mkoani Mwanza wakijitambulisha wakati wa uzinduzi wa ofisi ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza (Chadema).
Akina mama wa Chadema wakiwa katika uzinduzi wa ofisi ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza (Chadema).
Bendera za Taifa na Chadema zikipandishwa wakati wa uzinduzi wa ofisi ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza (Chadema).
Akina Mama wa Chadema Mkoani Mwanza wakimlaki Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake Chadema Taifa BAWACHA na Mbunge Viti Maalumu Taifa Grace Tendega wakati wa Uzinduzi wa ofisi ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza (Chadema).


Imeandaliwa na George Binagi-GB Pazzo @BMG