Thursday, April 5, 2012

ZIDANE AWAPOKEA SIMBA ALGERIA

Hoteli ya Mwanasoka Maarufu Zinedine Zidane ndiyo iliyokipokea Kikosi cha Simba.
KIKOSI kamili cha Simba kiliwasili jijini Setif jana majira ya saa saba na nusu mchana saa za hapa (saa tisa na nusu saa za huko), baada ya safari ndefu ya kutoka Algiers.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga amesema kutoka mjini Setif kwamba klabu yake iliwasili Algeria juzi lakini ilishindwa kwenda Setif kutokana na kukosa usafiri wa ndege, na kukataa usafiri wa basi ulioandaliwa na wenyeji wao.
 
Wakati wenyeji wakidai kwamba usafiri wa kutoka Algiers ilikolala Simba hadi Setif ni masaa matatu, jana Simba ilitumia takribani dakika 45 kwenda mji wa Bizaya (Bezaia) kwa usafiri wa ndege na kisha kupanda basi kwa muda wa karibu masaa mawili na nusu hadi kufika Setif.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika benchi la ufundi la Simba leo klabu itafanya mazoezi yake katika Uwanja wa Mei 8, 1945 majira ya saa 12 jioni kwa saa za hapa.
 
Uwanja huo ndio utakaotumika kwa ajili ya mechi ya Kombe la CAF baina ya Simba na Setif iliyopangwa kufanyika kesho Ijumaaa saa 12 jioni kwa saa za hapa sawa na saa mbili usiku kwa saa za Tanzania.
 
Msafara wa Simba umekuwa kivutio kikubwa nchini Algeria, kutokana na unadhifu wa wachezaji wake ambao wote wamevaa suti za wabunifu zinazowatofautisha na abiria wote wengine kwenye viwanja vya ndege ambako timu imepita.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Algeria, mechi ya kesho itachezeshwa na waamuzi kutoka Tunisia huku Kamisaa wa mchezo akiwa anatokana nchini Gabon.

No comments: