Thursday, January 24, 2013

APENDEKEZA KATIBA IMPUNGUZIE MAMLAKA YA KUFANYA UTEUZI WA VIONGOZI.

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ametaka Katiba Mpya impunguzie Rais madaraka hasa katika nafasi ya uteuzi.
Kauli hiyo ya Pinda inapingana na ile iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kuhusu Katiba Mpya ambaye aliiambia Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba madaraka ya Rais yasiguswe akisema kama atanyang’anywa, atashindwa kuongoza nchi.
Balozi Sefue alisema nafasi ya Rais inapaswa kuwa imara na yenye uwezo wa kuwaunganisha Watanzania wote.

“Asilimia kubwa ya Watanzania, wamekuwa wakipendekeza Rais apunguziwe madaraka aliyonayo, jambo ambalo linaweza kuleta hatari mbeleni, suala hili linatupasa kuwa nalo makini,” alisema Balozi Sefue na kuongeza:
“Tusiwe wepesi wa kutamka maneno bila ya kutafakari hasara na faida zake, tunapaswa kutambua taifa letu lenye miaka 51 ya Uhuru bado maskini, kuna mataifa yenye miaka 200 hadi 400, lakini kamwe hayathubutu kumpunguzia Rais madaraka.”
Hata hivyo, jana Pinda aliiambia tume hiyo ya Mabadiliko ya Katiba: “Kuna haja ya kumpunguzia Rais madaraka kwani amekuwa na mzigo mkubwa wa kuongoza Serikali. Kitu kikubwa ambacho ningependa kiangaliwe kwenye Katiba Mpya kwa upande wa madaraka ya Rais ni katika uteuzi wa viongozi mbalimbali.”
“Nimetaka Katiba Mpya impunguzie mzigo Rais kwani amekuwa na kazi nyingi sasa ni vyema angepunguziwa mzigo huo hasa katika masuala ya uteuzi wa viongozi.”
Pinda alitoa mfano kwamba katika kazi ya uteuzi wa viongozi, Makamu wa Rais anaweza kumsaidia kazi hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine ambavyo Katiba itaviainisha.

Mbali na hayo, Pinda alitaka pia Katiba Mpya izuie wabunge kuwa mawaziri na Serikali za Mitaa ziwekewe mfumo sahihi wa kujiendesha na kuwe na tume itakayoshughulikia masuala ya Muungano, lakini akataka Muungano ubaki wa Serikali mbili.Mwananchi.

No comments: