Sunday, February 17, 2013

Pombe ‘feki’ zafurika, wanywaji hatarini.

MAELFU ya wanywaji wa pombe hasa pombe kali, wako katika hatari kupata magonjwa ya ini na upofu wa macho kutokana na kufurika kwa pombe ‘feki’ katika maeneo mbalimbali nchini ambazo huzinywa.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili katika mikoa mbalimbali nchini, umebaini kuwa watu hao hununua pombe hizo feki, zinazotengenezwa kienyeji vichochoroni na kuwekwa katika chupa na ‘viroba’ zilizo na nembo za kampuni halisi zi nazozalisha pombe hizo.
Pombe hizo feki huuzwa katika hoteli, baa, grosari, vibanda vya pombe za kienyeji na meza za wafanyabiashara ndogondogo zilizogaa maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwamo masoko na vituo vya mabasi.
Uchunguzi huo umebaini kuwepo kwa mtandao wa vigogo, wanaojihusisha kuhujumu viwanda na kampuni zinazotegeneza pombe hizo nchini kwa kutengeneza pombe feki.
Pombe zinazotengenezwa kienyeji na mtandao huo wa wafanyabiashara wakubwa na baadhi ya watu waliokaribu na vigogo wa siasa nchini ni pamoja aina ya Whisky, Vodka, Valuer, Gin, Konyagi na Kiroba Original.
Uchunguzi umebaini kuwa kazi hiyo ya kutengeneza pombe feki inafanyika katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro na Singida.
Jijini Dar es Salaam kazi hiyo inafanyika katika maeneo ya Manzese, Tandika na Kitunda.
Mmoja wa wakazi wa Dar es Salaam, John Kwilasa mkazi wa Mbezi Beach Mtaa wa Yekeyeke alisema kuwa baadhi ya wanawake huuza konyagi feki hasa za paketi maarufu kama viroba.
“Siku hizi kuna konyagi feki zinauzwa pale mtaani kwetu. Kuna siku nimeagiza nikaletewa kiroba, nilipokunywa nikashangaa kusikia ladha nyingine. Nilipowauliza wenzangu nikaambiwa huwa kuna pombe feki, niwe makini,” alisema Kwilasa.
Mfanyabiashara Chriss Martin anayefanya biashara katika miji ya Mwanza, Moshi na Dar es Salaam, alisema kuwa kuzagaa kwa pombe hizo ni matokeo ya rushwa katika vyombo vya usimamizi wa bidhaa.
“Juzi juzi nilikuwa Dar es Salaam, nikaagiza pombe aina ya gordon’s na nilipoiweka tu mdomoni nikagundua ni feki, maana hata ladha siyo yenyewe. Niliimwaga na hili ni tatizo, liko miji mingi tu nchini,”alisema.
Uchunguzi unaonyesha kuwa pombe kali zinazotengenezwa kienyeji na kujazwa kwenye chupa za vinywaji halisi ni zile ambazo hupendwa na wanywaji nyingi kati ya hizo zikiuzwa kwa bei nafuu.

No comments: