Saturday, March 16, 2013

MAADHIMISHO YA WIKI YA MAJI KITAIFA MKOA WA LINDI.

TAARIFA YA KAIMU MKUU WA MKOA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA WIKI YA MAJI KITAIFA TAREHE 16-22/2013 MKOANI LINDI.
Ndugu Waandishi wa Habari na Wananchi wote wa Mkoa wa Lindi;
Napenda  kuwafahamisha kuwa Mkoa wetu umepewa heshima na Wizara ya Maji kuwa Mwenyeji wa maadhimisho ya 25 ya Wiki ya Maji Kitaifa yatakayo anza tarehe 16 Machi, 2013 na kufika kilele tarehe 22 Machi, 2013.
Shukrani
Napenda kuishukuru Wizara ya Maji kwa kutupa heshima ya kuwa wenyeji wa maadhimisho ya Kitaifa ya 25 ya Wiki ya Maji.
Aidha, navishukuru sana Vyombo vya Habari kwa kufika katika mkutano huu na kuwa tayari kutangaza mafanikio yaliyowekwa katika Sekta ya Maji.
Naamini maadhimisho haya yatakuwa chachu kwa wadau mbalimbali kuchangia kwa hali na mali katika ujenzi, uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji Mkoani wa Lindi.
Utangulizi;    
Kila mwaka kuanzia mwaka 1988, Tanzania imekuwa ikiadhimisha Wiki ya Maji kuanzia tarehe 16-22 Machi kwa kuwahusisha wananchi na wadau wote wa maji. 
Kilele cha maadhimisho huwa ni tarehe 22 Machi ambayo siku hiyo inafahamika Kimataifa kuwa ni Siku ya Maji Duniani kwa mujibu wa Azimio Na. 193/47 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Uzinduzi utafanyika tarehe 16 Machi 2013 katika Kijiji cha Mtandi Wilaya ya Kilwa na Kilele cha Maadhimisho kitakuwa tarehe 22 Machi 2013 katika Manispaa ya Lindi kwenye Uwanja wa Ilulu.  Mgeni Rasmi katika Kilele cha Maadhimisho atakuwa ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. JAKAYA MRISHO KIKWETE.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji ya mwaka  huu yataongozwa na Kauli Mbiu isemayo “MWAKA WA USHIRIKIANO WA MAJI KITAIFA”.
Madhumuni ya Maadhimisho;
Madhumuni ya Maadhimisho ya wiki ya maji ni  pamoja na:-
Kuwaelimisha wananchi kuhusu Sera ya Maji na majukumu yao katika kuitekeleza.
Kutathmini maendeleo ya Utekelezaji wa Programu ya  Maji, hali ya huduma ya maji na usafi wa mazingira na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma na uhifadhi wa rasilimali za Maji.
Kuhamasisha wananchi na wadau wengine kushiriki  katika kupanga, ujenzi, uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji na usafi wa mazingira.
Kujenga mshikamano miongoni mwa wadau mbalimbali wa Sekta ya Maji.
Kutoa ujumbe kwa wadau  kuhusu Kauli Mbiu ya Wiki ya Maji na Siku ya Maji Duniani.
Madhumuni  hayo yanalenga kuboresha  utoaji wa huduma  ya Maji, Usafi na Uhifadhi wa Mazingira, pamoja na usimamizi na utunzaji wa rasilimali za Maji nchini (vyanzo vya maji na miundombinu ya kufikisha huduma ya maji kwa watumiaji).
Maandalizi ya maadhimisho ya Wiki ya Maji mwaka 2013;
Maandalizi ya Maadhimisho ya Wiki ya Maji yanaendelea vizuri na uzinduzi na kilele cha maadhimisho kitawahusisha viongozi wa Kitaifa. 
Maadhimisho ya mwaka 2013 yanakusudia kuwashirikisha wananchi katika:-
kupanga, kujenga, kuendesha na kufanyia matengenezo miradi ya maji na kuimarisha usafi wa mazingira,
kutunza vyanzo vya maji na kuwaelimisha wananchi juu ya matumizi endelevu ya rasilimali za maji.
Matukio haya yataenda sambamba na kutoa ujumbe (maudhui) wa  Siku ya Maji Duniani ya mwaka 2013 ambao ni  “MWAKA WA USHIRIKIANO WA MAJI KITAIFA”.
Shughuli zitakazofanyika katika Wiki ya Maji hapa Mkoani Lindi ni pamoja na:-
Kuzindua miradi 3 ya Maji vijijini ambayo ujenzi wake umekamilika.
Vijiji hivyo ni Mtandi (Wilaya ya Kilwa), Rondo Mnara (Halmashauri ya Wilaya ya Lindi) na Luchelegwa (Wilaya ya Ruangwa).
Miradi hii imetekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji na wadau mbalimbali.
Kuzindua Mradi wa Uboreshaji Huduma ya Maji katika Mji wa Lindi kutoka chanzo kilichopo katika eneo la Kijiji cha Sinde.
Kutakuwa na Mikutano ya Hadhara maeneo yote ya Uzinduzi
Miradi yote itakayozinduliwa itawanufaisha wananchi wapatao 134,108.

Kugharamia Maadhimisho;
Ili kuweza kugharamia maadhimisho ya Wiki ya Maji mwaka 2013, Wadau mbalimbali wameombwa kutoa michango ya hali na mali ili kufanikisha maadhimisho haya.
Maadhimisho ya kitaifa  ya Wiki ya Maji yanagharimiwa na Wizara ya Maji , Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mamlaka za Maji Safi na Maji taka nchini, Halmashauri, Taasisi na Mashirika mbalimbali ya Kiserikali na yasiyo ya Kiserikali na Watumiaji Maji.
Napenda kuchukua fursa hii kuwaomba wadau wote kutoa michango ya hali na mali ili kuweza kufanikisha maadhimisho haya ya Wiki ya Maji Kitaifa yatakayofanyika hapa Mkoani kwetu mwaka huu wa 2013.

Wito kwa Wananchi wa Lindi;
Nitoe wito kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi kuwapokea na kuwakaribusha wageni wote ambao watakafika Mkoani kwetu kwa nyakati mbalimbali katika Maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani. Kipekee ninawaomba Wananchi/Wakazi wa Manispaa ya Lindi kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania atakapowasili tarehe 21 Machi, 2013 na kuendelea kuwa nae mpaka siku ya Kilele cha Maadhimisho katika Uwanja wa Ilulu tarehe 22 Machi, 2013.


Ahsanteni kwa kunisikiliza.


No comments: