Monday, July 15, 2013

UKUMBUSHO KWA WAISLAMU NA DARSA KWA WENGINE.

Muhammad bin Siriyn amesema, "Abu Huraryah amesimulia Hadiyth hii na akasema: "Huyu ni mama yenu enyi wana wa maji ya mbinguni" (yaani Waarabu kizazi cha Ismaa'iyl عليه السلام, mwana wa Haajar ambaye ndiye aliyesababisha maji ya Zamzam). [Fat-h Al-Baariy 6:447, Muslim 4:1840]

Mke wa Ibraahiym عليه السلام Sarah, alikuwa tasa. Na Ibraahiym عليه السلام alikuwa anazeeka na nywele zake zikatawaliwa na mvi baada ya kuita watu miaka mingi katika dini ya Allaah. Sarah akafikiria kwamba yeye na Ibraahiym عليه السلام wako katika upweke kwa vile hawakupata mtoto. Kwa hiyo akampa mumewe mtumwa wake Haajar amuoe. Haajar akamzaa Ismaa'iyl عليه السلام ambaye ndiye mtoto wa mwanzo wa Ibraahiym عليه السلام.

Siku zikapita na Ibraahiym عليه السلام akawa na furaha ya kupata mtoto, lakini Sarah akawa na wivu sasa na Haajar, ingawa yeye mwenyewe ndiye aliyempa Ibraahiym عليه السلام Haajar amuoe. Wivu huo ukamfanya Haajar awe anajificha ili Sarah asimuone anapokwenda kwa mumewe. Akawa ni mwanamke wa kwanza kufunga mkanda kuficha alama zake kama ilivyotajwa katika Hadiyth ndefu kutoka kwa Al-Bukhaariy iliyopokelewa na Ibn 'Abbaas kwamba "Haajar ni mwanamke wa mwanzo kutumia mkanda".

Makusudio hapo ni mkanda kiunoni kuzuia nguo yake ndefu inayoburuza ardhini isiache alama apitapo (ikaja ikajulikana na Sarah kuwa kapita). Inasemekana kuwa wakati huo wanawake walikuwa wakivaa nguo ndefu zinazoburuza. Na hii inaonyesha jinsi stara ilivyokuwa kwa wanawake tangu wakati huo.

Pia katika masimulizi kwenye Sahiyh Al Bukhaariy anasema, ''Wakati Nabii Ibraahiym عليه السلام alipomuoa Haajar na akamzalia Ismaa'iyl عليه السلام, mkewe wa mwanzo, Sarah, akapata wivu na akaapa kuwa atamkata mwili wake vipande vitatu, hivyo Haajar akajifunga mkanda kiunoni mwake na kukimbia huku akiburuza vazi lake nyuma yake ili kufuta alama za nyayo zake ili Sarah asiweze kujua alipoelekea. (Al Bukhaariy - Kitabu cha Visa Vya Mitume, hadiyth namba 3364)

Na Allaah Anajua zaidi.

No comments: