Saturday, July 27, 2013

VIONJO VYA MWEZI MTUKUFU, Ifuatayo ni Dondoo (excerpt) ya kitabu cha Salim Boss kiitwacho “Wao Ima ni Waerevu Mno au Wajinga Mno” chenye kurasa 672 zote zimechapishwa kwa rangi (full colour). Kinunue kwa Tshs 17000 na Kshs 900. Ni tarjama ya kitabu kilichouzika sana kiitwacho “They are Either Extremely Smart or Extremely Ignorant” *****Assilmi alilelewa katika familia ya kizungu ya Marekani, Mabaptisti wa kusini mwa Oklahoma. Alikuwa mwanaharakati wa siasa kali kupigania na kutetea ukombozi, haki, na usawa wa wanawake. Assilmi alikuwa pia ni mwanahabari.
Kisa chake cha kuvutia kilianza pale kompyuta ya chuo kikuu ilipokosea na kumsajili kuwa katika darasa linahusika na masuala ya tamthilia na maigizo. Kule alikutana na wanafunzi Waislamu. Alijihisi ana jukumu la kutimiza. Katika jaribu zake za kuwabatiza wale wanafunzi waarabu wa kiislamu, aliwahubiria sana kwa kuwaeleza “Mtaungua motoni tena milele kama mkikataa kumkubali Yesu kama mwokozi wenu.” Akiendelea kujaribu kuiteka mioyo yao Assilmi alisema: “Niliwaelezea vipi Yesu alivyowapenda na alikufa katika msalaba kwa ajili ya dhambi zao, na walichotakiwa kufanya ni kumkubali tu moyoni mwao.” Alipoona mahubiri yake yanagonga mwamba, yasilete tija yoyote akaamua kuisoma Qur’an ili apate mwangaza kidogo wa kiislamu ambao ungemsaidia kuwaelewa Waislamu vizuri ili awabadili kirahisi kuingia katika Ukristo. “Nikapatwa na mshtuko mkubwa,” Assilmi alisema, akimaanisha aliyoyaona kutoka katika Qur’an. Na ndoto za kuwabadili wenzake zikaishia kumbadilisha yeye mwenyewe.
Assilmi aliusoma Uislamu vizuri na akasema: “Kwa kipindi cha miaka miwili nimesoma ili nijaribu kuwabadili Waislamu waje kwenye Ukristo.” Katika kipindi hiki alisoma Qur’an yote vizuri, Sahih Muslim, na vitabu vyengine 15 vya kiislamu. Kiufupi aliirudia kusoma Qur’an. Wakati alipoisoma Qur’an, Assilmi akakutana na maswali ambayo yalijibiwa na rafiki yake wa chuo Abdul-Aziz Al-Sheikh. Baada ya kuugundua ukweli kutoka katika Uislamu, Assilmi hakuwa na jengine isipokuwa ni kukubali kwa ulimi na kukiri kwa moyo kuwa “Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu (Allah) na Muhammad ni Mtume wake.” Hii ilikuwa tarehe 21 Mei 1977. Akachagua jina la Amina Assilmi. Mwanzoni aliahidi hatofunika nywele zake na kama mmewe akioa mke mwengine basi atamhasi. Hata hivyo, baada ya kuzama kwa kina katika dimbwi la maarifa ya Uislamu akajikuta akivaa hijaab. “….hata nikaja kuwa mtetezi wa ndoa za mitara (polygyny),” Aliongeza, “Nilijua kama Allah karuhusu jambo hilo, lazima kutakuwa na faida kubwa ndani yake.”
Baada ya kusilimu, Amina alikimbiwa na marafiki wake wengi, kwani ‘hakuwa mtu mzuri tena kwao’. Dada yake ambaye ni ‘mtaalmu wa afya ya ubongo na akili’, alifikiri amechanganyikiwa hivyo alijaribu kumpeleka katika vituo vya kupima akili. Kusikia kusilimu kwake, baba mzazi wa Amina, alijaza bunduki yake kwa risasi mbioni kumtafuta amuue. “Ni bora afe…” Baba alisema. Siku alipoanza kuvaa hijab, dada huyu ambaye alishatunukiwa zawadi ya uandishi wa habari alifukuzwa kazi. Na baada ya kujitangaza wazi kuwa yeye sasa ni Muislamu, alipewa talaka na mme wake. Kisa kusilimu tu, akakataliwa kukaa na watoto zake wawili wadogo ambao aliwapenda sana na kihaki yeye ndiye aliyepaswa kupewa watoto hao. Kiukweli hakimu wa serikali hakumpa machaguo mazuri kabla ya kutoa hukumu: Ama akatae Uislamu na apewe watoto au aendelee na Uislamu wake huku akiwakosa watoto. Kitu kilichomuumiza zaidi ni kujua kutoka kwa madaktari kuwa hataweza kupata mtoto mwengine kutokana na matatizo fulani fulani. Lakini bado akaamua kubaki na Uislamu. Watoto wake wadogo – kamoja kavulana na kamoja ka kike- wote walipelekwa kwa mme wake wa mwanzo. Maumivu yakazidi kutoka moyoni hadi mwilini kwani alisema, “Nimepigwa na wakati sijawahi kunyanyua mkono wangu kumpiga yeyote.”  Mabadiliko katika maisha yake yakazidi kuonekana pale alipojaribu kufikisha cheki katika benki yake huku akiwa amevaa niqaab (akifunika uso kasoro macho) na mlinzi wa benki alimuoneshea bastola yake akijitayarisha kummaliza nayo iwapo atasogea hata hatua moja.
Mashaallah!
Japokuwa familia yake alimkasirikia mwanzoni, aliendelea kuwasiliana nao na kuwaitikia kwa heshima, taadhima na uvumilivu. Maisha yake mapya yakambadili na kuwa mtu mwema, kitu kilichopelekea hadi familia yake kumkubali na kumpenda. Ile kani isiyoonekana ya uzuri wa Uislamu kutoka kwa Assilmi ikaivuta familia yake kuuingia Uislamu. Wa kwanza katika waliyosilimu alikuwa ni bibi yake ambaye alikuwa na zaidi ya miaka 100. Aliyefatia ni yule aliyetaka kumuua aliposikia mwanawe kawa Muislamu. Baada ya miaka kadhaa mama yake naye akaungana nao katika Uislamu. Dada yake ambaye alifanya juhudi ili awekwe katika hospitali za vichaa akasilimu na yeye. Mwanawe mkubwa, Whittney, baada ya kufika miaka 21, aliukubali Uislamu vile vile. Miaka 16 baada ya kuachana, mume wake wa mwanzo naye akawa Muislamu. “Ndugu zangu wengi wanakuwa Waislamu kutwa kuchwa,” Alisema.
Dah!
Assilmi baadae aliolewa na mtu mwengine, na japokuwa matabibu walimueleza hataweza kupata mtoto, Mwenyezi Mungu alimbariki na akapata mtoto mwengine wa kiume. Aliachishwa kazi kutokana na kuvaa hijab, lakini sasa yeye ni rais wa Baraza la Kimataifa la Wanawake wa Kiislamu (International Union of Muslim Women). Amekuwa akihitajika sana duniani kote kufanya mihadhara mbali mbali.
Amina kwa sasa anafuraha na karidhika kuwa Muislamu. Anasema:
“Nina furaha sana kuwa Muislamu. Uislamu ndio maisha yangu. Uislamu ndio mapigo yangu ya moyo. Uislamu ndio damu inayosafiri katika mirija yangu ya damu. Uislamu ndio nguvu zangu. Uislamu ndio maisha yangu bora na mazuri. Pasina na Uislamu mimi si chochote si lolote. Na kama Allah asingeniangalia kwa jicho la huruma, nisingeweza ishi.”
Naam!

No comments: