Saturday, August 10, 2013

MWANDISHI WA HABARI MWINGEREZA ALIYETEKWA NA TALIBAN ASIMULIA YALIYOMKUTA.

Jazaakh Llah Khaira.
Karibu na jiji la Jalalabad, mnamo mwaka 2001 wakati utawala wa Kiislam wa Taliban ulivyokuwa hatamuni. Hata kamera zilipigwa marufuku katika utawala huo. Taliban walikuwa washatangaza vita tukufu kwa yeyote mpinzani wao. Mwandishi habari wa Kiengereza akiwa amevalia Burka huku akiendesha punda wake alikuwa tayari kuchukua jukumu zito la kisiri katika sehemu hii ya Afghanistan iliyokuwa ikitawaliwa na Taliban. Alijiingiza katika nchi kinyemela, hakuwa na kitabu cha utambulisho wakati wa kusafiri (paspoti) wala viza. Alikuwa ni jasusi wa kimarekani? Hakuna ambae aliweza kusema na kugundua mpaka pale yasiyotegemewa yalipotokea. Kamera ambao alijitahidi kuificha kwa ustadi katika burka lake ilimdondoka na kuonekana na askari wa kitaliban ambae hakuwa mbali nae. Akatumia siku sita katika makao makuu ya usalama wa taifa kule Jalalabad kabla ya kupelekwa katika (chuo cha mafunzo) gereza la Kabul ambapo kitanda kilikuwa ndani ya selo chafu yenye kachumba kadogo kisicho na maji; fikra zake zilimtuma kufanya matayarisho ya mwili wake kwa ajili ya zana mbali mbali za mateso kama za umeme, bakora, na hata kupigwa mawe mpaka kufa.
Labda alifikiri anawazidi ujanja wataliban! Kwani Yvonne aliahidi kuisoma Qur’an kama ataachiwa huru. Kule kwao Uingereza, mmewe aliangua kilio kutwa kucha pindi tu aliposikia kuwa Yvonne yuko katika mikono ya wataliban.…  “Taliban ni utawala wa siasa kali, nadhani watafikiri ameenda kule kwa ajili ya kupeleleza.” Alisema huyo mumewe.
Ahadi ya Allah Inatimia.
Yvonne Ridley alizaliwa mwaka 1968 huko Stanley, County Durham, Uingereza. Alikulia makuzi ya Kiprotestanti katika kanisa la Uingereza. Alikuwa mwimbaji mzuri tu kanisani na pia mwalimu wa mafundisho kwa watoto kanisani katika kijiji chao hicho kilichopo kaskazini mwa nchi hiyo. Baadae, akawa mwandishi wa habari katika gazeti la Sunday Express. Kwa miaka ipatayo kumi Yvonne amekuwa akifanya kazi katika magazeti mbalimbali yenye hadhi kama vile The Sunday Times, The Observer, Daily Mirror na Independent.
Mwanahabari huyo ambaye alishawahi kupata tuzo, pia amefanya kazi kama mrusha matangazo, prodyuza na pia mtangazaji katika vipindi na mashirika tofauti kama BBC TV na redio, CNN, ITN na Chalton TV akisafiri sana Afghanistan, Iraq na Palestina.
Tukirudi katika tukio lake akiwa mikononi mwa Wataliban, Yvonne Ridley akaanza kuwa mkaidi. “Nikawa mbaya kwa walioniteka, niliwatemea mate, mkaidi na nikagoma kula. Sema kweli sikuvutiwa na Uislam hata kidogo mpaka pale nilipokuwa huru kutoka katika mikono hii.” Alisema. Mmoja kati ya wale waliomteka alimuomba awe Muislam akakataa, lakini hata hivyo akaahidi kama akiachwa huru ataisoma Qur’an. “Nilitoa ahadi kwa sheikh wakitaleban kuwa nitausoma Uislam kama nikiachiwa. Nilisema hayo baada ya kuulizwa kuhusu utayari wangu katika kuukubali Uislam na nikahofia kutoa jibu la ‘ndio’ au la ‘hapana’ kwani iliwezekana majibu yote yakaeleweka vibaya na kutafutiwa sababu tu ya kupigwa mawe na kufa.” Siku kadhaa baadae Yvonne aliachwa huru bila kuumizwa kwa amri ya Mullah Omar, kiongozi wa kiimani wa Taliban ambaye ni mwenye jicho moja.
Kuhusu elimu na imani yake ya awali kuhusu Uislam, Ridley alisema “Sijui kitu kwani hata nikielezea nijuayo sidhani kama naweza jaza kile kikaratasi cha stempu. Ila ningeweza kuelezea yale yote yaitwayo maovu na ubaya wa Uislam kama unyanyasaji wa kijinsia, vipi ilivyo dini chafu na mbaya iliyojaa siasa kali.” Lakini baada ya kuisoma Qur’an ‘katiba impayo haki mwanamke (magna carta for women)” kama alivyoiita mwenyewe, Yvonne akaamua kusilimu mwaka 2003 katika majira ya joto, ikiwa ni miaka miwili na nusu tu baada ya kukamatwa kwake. Aliacha vileo mwaka mmoja kabla ya kusilimu. Na kwa kweli huwa anajisikia fahari sana pale asikiapo mtu wa kwanza kusilimu alikuwa ni mwanamke naye ni mke wa Mtume (Khadijah bint Khuwailid) na asikiapo kuwa shahidi (aliyekufa kwa ajili ya dini) wa kwanza pia alikuwa ni mwanamke (Sumayya). Yvonne anapenda kuvaa hijab. “Inaieleza dunia kuwa mimi sasa ni Muislam: usinipige, usiniongeleshe ovyo, usinialike katika vilevi wala nyama ya nguruwe; na kama ukihitaji tuzungumze yatupasa kuzungumza mambo ya msingi tu. Na mpaka sasa sikumbuki lini ilikuwa siku ya mwisho mtu kunitania utani mchafu, napenda waendelee hivyo….” Alisema.
Bilashaka wenye kufikiri wanafikiri.
Akishangazwa na ukweli wa Qur’an, alisema, “Niliathirika sana na nilichokuwa nakisoma- hakuna hata kanukta kalichobadilishwa (katika Qur’an) kwa miaka zaidi ya 1400 sasa.” Akilinganisha haki za wanawake kutoka katika Qur’an na zile wanazoziita haki kule Magharibi, Ridley alinena, “Kitu cha kwanza kukifatilia katika Qur’an kilikuwa ni sheria za ndoa, talaka na mali. Nikashangazwa sana. Nilifikiri (Qur’an) imeandikwa na wakili wa sheria kutoka Hollywood (eneo Marekani maarufu na mahsusi kwa ajili ya matengenezo ya filamu). Kwa kweli, ni kutoka humu ndio wamepata wanayoyadai.” Katika kutimiza ahadi yake aliyoitoa kule gerezani, ilimbidi apate kazi ya kuzunguuka kwa wanazuoni mbali mbali waaminikio wa Kiislam kwa ajili ya utafiti zaidi wa Uislam. Alikwenda kwa dokta Zaki Badawi kwa ajili ya ushauri na ufafanuzi; akagaiwa vitabu vingi vya sheikh maarufu Abu Hamza Al-Masri ambae alionana nae baada ya wote kuhutubia katika majadiliano (debate) ya pamoja kule Oxford.
Pia ameweza kumsikiliza na kuonana nae Dkt. Muhammad Al-Massari, kumuelezea masuala kadhaa ya Uislam. Kuusoma kwake Uislam kulipelekea kuja kusema haya:
“Hii Qur’an imeweza kuandikwa jana kwa ajili ya leo. Inaweza kukaa pamoja na mwanaharakati yeyote wa mazingira, ni rafiki mzuri wa mazingira na ni wazo kuu kwa ajili ya karne hii ya 21, chakushangaza haijabadilika hata neno moja tangu iandikwe sio kama haya matabu mengine makubwa na mazito yanayotazamiwa kuja kuleta tija.”
Nahuu ndio Uisilamu.
Badiliko lake lilikumbana na mitihani na vikwazo vigumu, yote ni tu kwa kuwa ameamua kuwa muumini mzuri wa Uislam avaaye hijab. Kulikuwa na dereva wa taxi aliyesema, “Usiache bomu katika siti ya nyuma” na kuuliza, “Wapi ambapo Bin Laden amejificha?”
Ridley ameandika kitabu kilichobeba jina la In the Hands of Taliban (Mikononi Mwa Wataliban) kilichochapishwa na Robson Books huko Uingereza. Kitabu kingine alichotunga ni Ticket to Paradise (Tiketi Kuelekea Peponi). Baada ya kusilimu tu Ridley alienda kuhiji.akieleza yaliomsibu akiwa anahiji, Ridley alisema:
“Hija ni zoezi zuri na la kushangaza. Kwa yeyote ambaye bado hajabahatika kuhiji namuusia afanye hivyo upesi. Inakuonesha mizizi ya Uislam. Kwangu mimi jambo hili si la kusahaulika kamwe. Siku moja nilikuwa naharakisha kuwahi jamaa (swala kwa pamoja na waumini wengine) ya swala. Nikiwa napita katika mitaa yenye kona nyingi kuelekea Haraam (msikiti mtukufu wa Makkah). Walikuwa malaki kama mie tukiwahi kuielekea swala. Ikawa vurugu njiani kwa kweli- kwani kila mtu alikuwa akisukuma sukuma ili aharakishe kufika katika Haraam kwa muda. Ghafla pakaqimiwa kuwataarifu watu wawe tayari kwa swala, kila mtu alisimama na bila zogo watu wote wakajipanga katika mistari haraka. Nikaanza kufikiria hakuna jeshi lolote duniani lenye uwezo wa kujipanga vile kwa haraka.  Na hivyo nikabaki nafikiria jeshi la Allah tu na moyo wangu ukitabasamu kwa mimi kuwepo ndani yake. Macho yangu huwa yanajawa na machozi kwa kufikiri hili nililoshuhudia. Ilinifanya nifurahi kuwepo katika familia hii kubwa. Pale, kulikuwa na watu kutoka mataifa tofauti, lugha tofauti na rangi tofauti. Swala ikaanza, wote tulielewa na wote tuliungana katika muungano mzuri usio na fujo, zogo wala kelele. Ilinihuzunisha sana kugundua kuwa tutadumu vile kwa sekunde kadhaa tu, nikajiuliza kwanini tusiendelee Waislamu kuwa hivyo baada ya swala pia!”
Yvonne ni mwanzilishi wa Women in Journalism (Wanawake Wana-habari), promota wa haki za wanawake na pia ni mwanzilishi wa Stop the War Coalition (Muungano wa Vyama Kupinga Vita) na chama cha siasa cha RESPECT. Pia ni mjumbe katika umoja wa wanahabari wa taifa The National Union of Journalists, The Internatinal Federation of Journalists (Shirikisho la Wanahabari la Kimataifa) na The Society of Authors (Umoja wa Waandishi, Watunzi). Kwa sasa, anafanya kazi kama mtangazaji katika kituo cha televisheni kipatikanacho dunia nzima cha PRESS TV. Pia ni mwandishi katika kijarida cha kila siku chenye makao yake New York kiitwacho Daily Muslims. Kwa maneno yake mwenyewe akiongelea kuhusu kusilimu kwake, Ridley anajisifu kwa kusema “Nimejiunga na familia ambayo kwangu mimi naichukulia kama ndio kubwa zaidi kwa sasa duniani bila kusahau ndio familia bora zaidi pia. Kama tukishikamana basi hakuna wa kutuzuia.” Baadhi ya masomo yake yapatikanayo kutoka katika intaneti ni kama ‘Conversion to Islam’ na ‘Journey to Islam’.
Kikazi zaidi.
Kuonesha kuumizwa kwake na haya mashambulizi ya kila siku katika kuusema vibaya Uislam, ameandika:
“ …Kwa sasa inauma na kuchosha kuona hapa Uingereza Jack Straw (aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje) akiielezea niqab (kujifunika uso kasoro macho tu) kama ni kikwazo kikubwa cha muingiliano katika jamii na hapo hapo waziri mkuu Tony Blair, mwandishi Salman rushdie na waziri mkuu wa Italia Romano Prodi wakiwa upande wake. Nikiwa nimepitia pande zote mbili, nakwambieni, wengi wa wanasiasa na wanahabari wakimagharibi ambao wanaonesha kuchukizwa na unyanyasaji wa wanawake katika maeneo ya Waislam hawajui walisemalo. Wanaongelea kujifunika, ndoa za watoto, ukeketaji wa wanawake, mauaji matukufu, na ndoa za kulazimishwa na wanaanza kuulaumu Uislam kimakosa. Jeuri yao imezidiwa na ujinga wao. Hizi tamaduni na desturi za watu hazihusiani Abadan na Uislam. Ukiisoma Qur’an kwa makini utagundua kuwa kila kitu ambacho hao wajiitao wanaharakati katika nchi za magharibi wanakipigania kilikuwepo kwa Waislam wanawake miaka 1400 iliyopita. Wanawake katika Uislam wako katika daraja moja na wanaume katika ucha Mungu, elimu na umilikiji mali. Na hii zawadi ya mwanamke kuzaa mtoto na kumlea tunalichukulia kama ni ushindi kwetu. Wakati Uislam unamgaia kila kitu mwanamke kwanini wanaume wa kimagharibi wapoteze muda wao kufatilia mavazi ya mwanamke wa Kiislam!? Hata mawaziri kama Gordon Brown na John Reid wamevalia njuga kuzungumzia niqab na wanatupia mbali yale yatokeayo hapo mpakani tu mwa Scotland (Uskochi) kwa wanaume kuvaa sketi….kipi ndio chafaa kutazamwa zaidi, kuhukumiwa kwa kuvaa sketi ndefu na umbo la matiti yako uliyoyarekebisha kwa operesheni au kuhukumiwa kwa kuangalia akili na tabia za mtu? Katika Uislam ubora unapatikana katika uchaji Mungu pekee, sio katika uzuri, mali, nguvu, cheo, au jinsia. Sikujua kama nilie au nicheke wakati waziri wa Italia; Prodi, alipoingilia majadiliano (debate) wiki iliyopita na kutangaza eti ni jambo la kawaida tu mtu kutovaa niqab kwani inafanya maingiliano katika jamii magumu. Huu kusema kweli ni upuuzi! Kama ni hivyo kwanini basi simu, barua pepe, ujumbe mfupi wa maneno, na nukushi vinatumika kila siku? Na huwezi ukakuta mtu anazima redio eti kwa sababu hamuoni mtangazaji.

No comments: