Saturday, September 19, 2015

ZITTO KABWE : HOJA YA UFISADI NI ENDELEVU.


Tanzania inaendelea kupoteza mabilioni ya fedha za umma kwa sababu ya ubadhirifu mbalimbali. Taarifa za Serikali zinaonyesha kuwa takribani 30% ya Bajeti ya nchi inaishia kwenye mifuko ya watu binafsi. Kashfa mbalimbali za ufisadi zimekuwa zikiibuliwa na kuleta mijadala mikali lakini watu wanaohusika hawachukuliwi hatua zozote. Jambo la kushangaza ni kwamba ajenda ya ufisadi imefifia katika uchaguzi tofauti na mwaka 2010. Haipaswi kuwa hivi kwani ufisadi ni Kansa inayotafuna Taifa letu. Lazima kuendelea kupambana dhidi ya ufisadi ili kuhakikisha nchi yetu inamaliza umasikini na kujenga dola la maendeleo ( developmental state ).
Juzi nilikuwa Mkoa wa Tabora. Wananchi wa Tabora wanalia Tumbaku yao kutonunuliwa. Tabora huzalisha Tumbaku nyingi zaidi kuliko mikoa yote nchini na kiungiza mapato ya fedha za kigeni zaidi ya usd 315 milioni mwaka 2014. Hata hivyo 10% ya mapato haya huibwa na vyama vya ushirika kwa kushirikiana na baadhi ya mabenki yanayosambaza pembejeo za kilimo. Ufisadi huu kwenye tumbaku hauzungumzwi ilhali ndio mustakabali wa wakulima wa tumbaku zaidi ya 1m katika mkoa wa Tabora.
Mwezi uliopita Serikali kupitia mfumo wa kuagiza mafuta kwa pamoja ilitoa zabuni kwa kampuni ya Augusta kutoka Switzerland. Zabuni hiyo ilipandishwa bei ( inflated prices ) kwa thamani ya usd 10m sawa na tshs 20 bilioni. Ndio maana wakati Dunia nzima bei ya mafuta imeshuka hapa Tanzania bei ipo juu kwa sababu wajanja wachache wamepeana Dili la uagizaji mafuta bila kufuata sheria ya manunuzi. Leo kila mwananchi anaumizwa na bei ya mafuta kwa sababu ya ufisadi huu.

Bado skandali za kifisadi zilizoibuliwa huko nyuma hazijapata majibu. Kwa mfano mpaka sasa bado kampuni ya IPTL inauza Umeme TANESCO licha ya Bunge kuazimia kuwa mkataba wake uvunjwe. Bado anayejiita mmiliki wa IPTL aliyetapeli nchi yetu  hajakamatwa mpaka Leo na waliochota fedha kutoka benki ya Stanbic hawajatajwa na kufikishwa mahakamani.
Vyama vinatamka kauli nyepesi nyepesi kuhusu mapambano dhidi ya ufisadi. Ni dhahiri kwamba lazima kurejesha agenda hii kwenye kampeni za uchaguzi kwa kila chama kusema kitafanya nini. Sisi ACT Wazalendo tumeweka kwenye ilani yetu hatua tutakazochukua kupambana na rushwa na ufisadi.

1) Kuipa mamlaka TAKUKURU ya kukamata na kuendesha mashtaka ya rushwa ( power to prosecute ) bila kusubiri kibali cha DPP. 
2) Kuanzisha idara ya rushwa kubwa kubwa ( Serious Fraud Office ) ambayo kazi yake itakuwa ni kupambana na ufisadi tu
3) Kutunga sheria ya Miiko ya Uongozi ili kudhibiti rushwa kwenye sekta ya umma na siasa. Mali za viongozi kuwekwa wazi na kukaguliwa na pale kwenye udanganyifu hatua kuchukuliwa ikiwemo kuvuliwa madaraka yao.

Ni imani ya chama chetu kuwa ajenda ya ufisadi itajadiliwa kwa kina kwenye kampeni na hasa kwenye midahalo ya wagombea Urais na viongozi wa vyama.

Nawaomba wananchi wa Kibaha muichague ACT Wazalendo ili iweze kuendeleza vita dhidi ya ufisadi na kusafisha nchi yetu dhidi ya wala rushwa. Naomba kura kwa Habib mchange kama mbunge, madiwani wa ACT wazalendo na mumchague mama Anna Mghwira kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Chagueni ACT Wazalendo ili kurejesha nchi yetu kwenye misingi.

No comments: